Sunday, May 11, 2014

WAFANYABIASHARA NCHINI WASHAURIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA BIASHARA UN

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imehamasisha jumuiya ya wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa za biashara katika Umoja wa Mataifa (UN).
Hayo yamesemwa na  Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, katika semina ya kuwahamasisha wafanyabiashara wa Tanzania kufahamu na kuzitumia fursa za biashara zinazojitokeza UN.

Semina hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni ilitayarishwa na TPSF kwa kushirikiana na kitengo cha manunuzi cha ofisi ya UN. semina hiyo ililenga kuwahamasisha wafanyabiashara, ili waweze kuwekeza kimataifa na kutanua wigo wa biashara.
Simbeye alisema kuwa  “Tumeleta wafanyabiashara wa Tanzania katika semina hii, ili kuweza kuangalia ni fursa zipi wanazoweza kuzipata katika zabuni za Umoja wa Mataifa,”
Aliongezea kuwa  Tanzania inashiriki kwa kiwango kidogo katika zabuni za UN, kitu ambacho kinawashangaza wadau mbalimbali hasa kutokana na mchango mkubwa wa Tanzania katika kuleta amani kwenye nchi nyingi duniani.
“Hatujafanya semina ya namna hii kwa miaka tisa sasa, kama inavyofanywa na nchi jirani kama Kenya na Uganda… kuna fursa nyingi za biashara na Umoja wa Mataifa,” alisema Simbeye.
Mkuu wa Idara ya Manunuzi  UN, Yavar Khan, alisema kuna kila sababu kwa Watanzania kushiriki kwa kiwango kikubwa katika kufanya biashara na umoja huo.
Ofisa Manunuzi Mwandamizi wa Ujumbe wa UN Sudan ya Kusini (UNMISS), Bruno Maboja, alisema mategemeo yao ni kuona kampuni za Tanzania zinashiriki katika biashara na umoja huo.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Powerade Coupons