skip to main |
skip to sidebar
Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) imetoa zaidi sh bilioni 20 kwa
wanawake wajasiriamali na vijana katika jitihada za kuwawezesha kukuza
mitaji na kuimarisha biashara zao nchini.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa benki hiyo, Margreth
Chacha, alipozungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini
Dar es Salaam kuwa katika kipindi cha chini ya miaka minne tangu benki
hiyo ianzishwe, maelfu ya wajasiriamali wanawake na vijana
wameshanufaika na mikopo ya kuendeleza biashara zao.
“Mikopo yetu kwa wajasiriamali hawa imekuwa kichocheo kikubwa
katika kupanua wigo wa biashara zao na marejesho ya mikopo hiyo kutoka
kwa wajasiriamali na vijana inaridhisha na kutia moyo,” alisema.
Chacha alisema benki yake imeona kwamba kuwawezesha wajasiriamali
wanawake na vijana kuna maana kubwa katika kuchangia maendeleo na
ukuaji wa shughuli za kijamii na uchumi nchini.
“Ni imani ya benki kuwa wanawake na vijana ni wachangiaji wakubwa
katika uchumi wa nchi, kwani wao idadi yao ni kubwa, hivyo endapo
watawezeshwa vilivyo basi wanasimama katika nafasi kubwa ya kubadilisha
uchumi,” alisema.
Kwa mujibu wa mkurugenzi mwendeshaji huyo, kiasi cha sh bilioni
17.6 zimetolewa kwa wajasiriamali na vijana kwa Mkoa wa Dar es Salaam,
sh bilioni 1.3 zimetolewa kwa wajasiriamali wa Dodoma na sh milioni
686 kwa wajasiriamali wa Mwanza.
“Wakati sasa tukiwa katika mpango kabambe wa kujitanua kila
sehemu hapa nchini, tayari benki yetu imeshatoa mikopo ya kiasi cha
shilingi milioni 178 kwa wajasiriamali na vijana mkoani Mbeya na kiasi
cha shilingi milioni 366 kwa wajasiriamali vijana mkoani Ruvuma.
“Wajasiriamali katika Mkoa wa Dodoma walijiunga katika vikundi na
mikopo yao waliitumia kununulia mashine za kukamulia mafuta ya alizeti
ambapo wale wa mkoani Mbeya walielekeza katika manunuzi ya mashine za
kulimia maarufu kwa jina la ‘power tillers’,” alisema.
Akifafanua zaidi, Chacha alisema vijana mkoani Ruvuma
wamewezeshwa kupata mitaji pamoja na kuwa hawakuwa hata na kianzio,
lakini benki imewawezesha.
“Vijana wapatao 80 wamewezeshwa kukopa
pikipiki, bajaj na magari madogo ya kubebea mizigo, na sasa wanazifanyia
biashara kubwa mkoani Ruvuma,” alisema.
0 comments:
Post a Comment