Mbunge wa Singida Kaskazini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Lazaro Nyalandu amejiuzulu nafasi yake ndani ya CCM na kujiuzulu nafasi
yake ya Ubunge kupitia (CCM) kwa kile alichodai hafurahishwa na mambo ya
kisiasa yanayoendelea nchini. Taarifa ambayo ameitoa leo Nyalandu amesema kuwa
ameamua kuachana na
CCM na sasa anaomba kuungana na
CHADEMA kama watapendezwa na yeye
kujiunga huko.
"Nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya Ujumbe wa Halmashauri
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani
ya Chama kuanzia leo, Oktoba 30, 2017. Halikadhalika, asubuhi ya leo
nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job Ndugai, Mb., barua ya kujiuzulu
nafasi yangu ya Ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kupitia tiketi ya
CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa vipindi vinne mfululizo tangu
nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 hadi Sasa" aliandika Nyalandu
"Nimechukua uamuzi huo kutokana na kutorishwa kwangu na
mwenendo wa hali ya Kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki
za Kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya
watanzania wenzetu, na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya mihimili
ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa
Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru
uliainishwa na kuwekwa bayana Kikatiba" alisisitiza
Mbali na hilo amesema kwa sasa anafikiria kujiunga na CHADEMA kama watakuwa tayari kumpokea ndani ya Chama hicho.
"Mimi naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM,
nikiwa nimekitumikia kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa
Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM
na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM TAIFA, kwani nimejiridhisha kuwa
kwa mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania
Sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa
hapo awali. Aidha, Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge
na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa
namna Moja au nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya miguu ya dola badala ya
chama kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa
maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
"Hivyo, kwa dhamira yangu, na kwa uamuzi wangu mwenyewe,
nikiwa na haki ya Kikatiba, natangaza kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM)
leo hii, na nitaomba ikiwapendeza wanachama wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) , basi waniruhusu kuingia mlangoni mwao, niwe
mwanachama, ili kuungana na CHADEMA na watanzania wote wanaopenda kuleta
mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa ki
demokrasia na uhuru wa mawazo.
"Nimemua kujiuzulu kiti Cha Ubunge, Jimbo la Singida
Kaskazini kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mwingine ili wananchi wapate
fursa ya kuchagua itikadi wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi
zenye changamoto lukuki nchini Tanzania. Ni imani yangu, kamwe
hayatakuwa ya bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya
Watanzania leo ili kwamba, sote kama Taifa tuingie kwenye mjadala wa
kuijenga upya misingi ya nchi yetu. Ni maombi yangu kwa Mungu kuwa haki
itamalaki Tanzania. Upendo, amani na mshikamano wa watu wa imani zote za
dini, mitazamo yote ya kiitikadi za kisiasa, na makabila yote nchini
uimarike. Tushindane ki sera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini
tubaki kama ndugu, na taifa lililo imara na nchi yenye maadili"
Alisisitiza Nyalandu


8:37 AM
0 comments:
Post a Comment