skip to main |
skip to sidebar
Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa
kwa Umma juu ya mwenendo wa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue
fever” hapa nchini.Ugonjwa huu umethibitishwa baada ya sampuli
zilizochukuliwa kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini
Dar es Salaam kupelekwa kwenye maabara yetu ya Taifa Dar es salaam na
kuthibitisha kuwa na virusi vya homa ya dengue mnamo mwishoni mwa mwezi
wa Januari 2014. Hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na
ugonjwa huuni 400 na Vifo 3. Kwa wiki iliyoshia tarehe 9 Mei 2014 ya
idadi ya wagonjwa waliogundulika mkoani Dar es salaam ni 60
(42-Kinondoni, 14-Temeke na 4-Ilala) na idadi ya wagonjwa waliopo wodini
mpaka sasa ni 13.
Aidha, mlipuko wa ugonjwa huu si mpya hapa nchini kwani uligundulika kwa
mara
ya kwanza mnamo Juni 2010 mkoani Dar es Salaam ambapo idadi ya watu 40
walithibitika kuwa na ugonjwa. Pia, kati ya mwezi Mei hadi Julai
2013,wagonjwa 172 walithibitishwa kuugua ugonjwa huu.
Homa ya Dengue
Homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes.
Dengue
in ugonjwa uliosambaa duniani katika nchi za ukanda wa joto. Takribani
asilimia 40 ya watu wote duniani wanaishi katika nchi zenye ugonjwa huu.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinathibitisha kuwa takribani
matukio milioni 5 ya Dengue yanatolewa taarifa kila mwaka. Watu laki 5
hulazwa hospitali kwa kuathirika na Dengue kali. Homa ya Dengue
imeshatokea katika nchi zipatazo 34 barani Afrika.
Hapa Afrika
Dengue ni ugonjwa unaojulikana kwa kiwango kidogo sana. Licha ya kwamba
milipuko ya kwanza imetokea tangu mwanzoni wa karne ya 19. Matukio ya
Ugonjwa huu yameongezeka Afrika tangu miaka ya 1980, matukio mengi
yakitokea nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika ikiwa ni pamoja na
Msumbiji, Somalia, Kenya, Komoro, Djibouti na Tanzania. Ikumbukwe kuwa
jina “Dengue” linatokana na neno “Dinga” la kiswahili linalolomaanisha
ugonjwa unaotakana na pepo yaani Kudinga pepo. Mabaharia wa Kispanish
walipokuja kwenye pwani ya Afrika Mashariki walirudi kwao na kuuita
“Dengue”.
Dalili za ugonjwa huu ni homa, kuumwa kichwa, maumivu
ya viungo na uchovu Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia katisiku ya 3
na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya dengue. Kwa wakati
mwinginedalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za
malaria, hivyo basi wananchi wanaombwa kuwa wakati wakipata homa
kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria ua la
ili hatua stahiki zichukuliwe.
Kuna aina 3 tofauti za namna ugonjwa huu unavyoweza kujitokeza iwapo mtu aking`atwa na mbu mwenye virusi hivi;
i.Homa
ya dengue (Dengue Febrile Illness): Aina hii huambatanana dalili kuu
tatu za homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo au
uchovu.Aidha, kwa Tanzania mpaka sasa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa
wamejitokeza na dalili hizi.
ii.Dengue ya damu (Dengue
Haemorrhagic Fever): Aina hii yahoma ya dengue huambatana na dalili za
mgonjwa kutokwa na damu kwenye fizi au puani, vile vile kutokwa na damu
chini ya ngozi.Iwapo mgonjwa huyu ataumia sehemu yoyote ni rahisi kwake
kupoteza damu nyingi kupitia kwenye michubuko.
iii.Dengue ya
kupoteza fahamu (Dengue Shock syndrome): Aina hii ya homa yadengue
huambatana na mgonjwa kupoteza damu nyingi ambayo hupelekea
mgonjwakupoteza fahamu. Dalili hizi zimeonekana kwa mgonjwa 1 kati ya
wagonjwa 400 waliokwisha kuthibitishwa kuwa na ugonjwa hapa nchini.
Kirusi
cha homa ya Dengue kinaambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa
kuumwa na mbu wa Jamii ya Aedes, na hasa Aedes aegypti. Mbu huyu anaishi
katika mazingira ya makazi ya binadamu. Huuma wakati ya mchana ndani ya
nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli, hususani majira ya asubuhi na
jioni kabla jua halijazama.
Mbu huyu anazaliana katika maji
yaliyotuama hasa kwenye vyombo vya nyumbani, makinga maji ya paa za
nyumba, matairi ya gari, ndoo, vikopo, na kadhalika. Kwa bahati mbaya
mbu huyu huweza kuzaliana katika vifaa vidogo vidogo ambavyo watu wengi
huvidharau. Hivi ni pamoja na makopo ya kuotesha maua, vikombe, vifuu
vya nazi, na kadhalika. Majani mapana yanayohifadhi maji ni mazingira
mazuri kwa kuzaliana kwa mbu huyu, hivyo maeneo ya bustani siyo ajabu
kuwa mahali pazuri kwa mbu hawa.
Ugonjwa huu hauambukizi kwa
kumhudumia mgonjwa au kugusa majimaji yanayotoka kwa mgonjwa. Homa ya
dengue inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na
kupatiwa matibabu ya haraka.Hakuna dawa maalumu ya ugonjwa wala chanjo
bali mgonjwa anatibiwa kutokana nadalili zitakazoambatana na ugonjwa huu
kama vile homa, kupungukiwa maji au damu. Endapo mgonjwa atachelewa
kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya dengue
Kuangamiza mazalio ya mbu
Fukia madimbwi ya maji yaliyotuamaau nyunyuzia viuatilifu vya kuua viluwiluwivya mbu kwenye madimbwi hayo
Ondoa
vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile: vifuu vya nazi,
makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo, nk.
Fyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu
Hakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama
Funika mashimo ya maji takakwa mfuniko imara
üSafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama
Kujikinga na kuumwa na mbu
Tumia viuatilifu vya kufukuza mbu “mosquito repellants”
Vaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu
Tumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu (kwa wale wanaolala majira ya mchana na hasa kwa watoto)
Weka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi
Hatua zinazochukuliwa na Wizara
(i)Hatua za Dharura
Uratibu
Timu
ya Taifa ya Maafa inayoshirikisha wadau mbalimbali ikiwemo wa
Halmashauri za Jiji na Wadau wa Maendeleo hukutana kila mara 2 kwa wiki
kutathmini mikakati ya dharura iliyowekwa.
Uelemishaji na Uhamasishaji wa Jamii
Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii ilitoa tamko la Serikali kwa nyakati tofauti
kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Dengue. Tamko la kwanza lilitolewa kwenye
vyombo vya habari tarehe 04 Februari 2014 na Machi 2014.
Kuendelea
kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote
wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara. Aidha taarifa hii pia
iinajumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa),
“Ukweli Kuhusu Ugonjwa“(Fact sheet), Mwongozo kwa watumishi wa afya wa
namna ya kuchukua sampuli. Vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga
na maambukizi ya ugonjwa huu vitatolewa.
Kuendelea kutoa elimu kwa
wananchi kupitia Radio, na Runinga. Aidha Wizara kwa kushirikiana na
Halmashauri za jiji wameendelea kutumia Maafisa Afyaikiwemo wa kata
kuwaelemisha wananchi namna ya kudhibiti ugonjwa kwakutumia vipaza
sauti, uongozi wa mitaa
Mafunzo kwa watalaam wa Afya
Kuendelea
kutoa elimu ya Afya kwa Watumishi wa Afya ikiwa pamoja na madaktari na
mafundi maabara namna ya kutambua ugonjwa huu. Aidha watumishi wa
hospitali za Muhimbili, Mwananyamala, Amana na Temeke wamekwisha kupewa
mafunzo haya na bado wanaendelea kupewa kupitia mikutano yao ya asubuhi
(Clinical meetings). Mafunzo haya pia yanaendelea kutolewa kwa vituo vya
chini kupitia Halmashauri
Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na mawasiliano
Kuimarisha
ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo vya kutolea huduma za afya
pamoja na mipakani kupitia mfumo wa saveilensi ya Wizara. Aidha, pamoja
na Mwongozo huu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa maelekezo kwa
Waganga wakuu wa mikoa na wilaya hapa nchini kutoa taarifa za wagonjwa
wa Dengue Fever kupitia taarifa za kila juma.
Kutoa miongozo ya
ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika maeneo ya mipakani kuhusu kutokuwepo
kwa aina yoyote ya vikwazo vitakavyowekwa kwa ajili kwa wasafiri. Aidha
maelekezo hayo yameainisha kuwa iwapo msafiri anayeondoka au kurudi
nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa
mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa
Kufuatilia kwa karibu
ongezeko la wagonjwa wenye homa isiyo kuwa ya malaria kwa Mikoa na
Wilaya zote nchini ili kuweza kufanya uchunguzi wa kina iwapo kuna
ugonjwa huu. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeshafanya utafiti
mkoani Kagera, Morogoro na Kigoma na kuthibitisha kuwa haijaadhirika na
dengue.
Kuanzishwa kwa vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu
katika Hospitali za Manispaa za jiji la Dar es Salaam (Mwananyamala,
Amana na Temeke). Aidha, Kituo cha ‘International School of Tanganyika –
IST’ kilichopo Manispaa ya Kinondoni na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
zinaendelea na ufuatiliaji wa ugonjwa huu. Aidha Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii itafungua pia vituo mkoani Tanga na Mtwara, mikoa
imayopakana na nchi jirani yaani Kenya na Msumbiji ambako ugonjwa huu
pia umetolewa taarifa.
•Kupeleka taarifa ya mlipuko huu Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kama mwongozo wa Kanuni za Afya za Kimataifa uvyaoelekeza.
Upimaji na Tiba
Kuimarisha
uwezo wa kutambua ugonjwa huu kwa kina kupitia maabara ya Taifa
(NHLQATC) iliyopo NIMR. Vile vile Wizara imepeleka vipimo sawia yaani
“Dengue Rapid Test Kits” kwa vituo vya Dar es Salaam kuimarisha
utambuzi. Vituo hivo ni pamoja na hospitali za Muhimbili, Amana,
Mwananyamala, Temeke Hospital, na IST kliniki. Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii imeagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuhakikisha vitendanishi hivi
vinakuwepo ili kurahisisha upatikanaji wake kwa Halmashauri zote na
kupelekwa kwenye vituo vya chini zaidi. Wizara imeagiza vipimo sawia 750
vya kunyongeza ambavyo tunatarajiwa kuvipata tarehe 22.5.2014
Wizara
imeweka utaratibu wa kuhakikisha vifaa Tiba vinapatikana wakati wote
katika vituo vyote kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa watakaogundulika na
kuwa na ugonjwa huu.
Udhibiti wa mbu na mazalia
Kudhibiti mbu
kupitia kwa kupulizia na kunyunyizia viuatilifu katika baadhi ya maeneo
yaliyoathirika katika mkoa wa Dar es salaam ambayo wametoka wagonjwa
wengi wa Dengue. Hii inalenga kuangamiza mbu wapevu na viluwiluwi.
Utafiti
Taasisi
ya Utafiti ya magonjwa ya Binadamu (NIMR) iko katika maandalizi ya
kufanya utafiti kuhusu dengue kwa kuangalia maaeneo makubwa mawili.
Ukubwa wa tatizo katika binadamu
Mbu
waambukizao ugonjwa wa homa ya Dengue- kujua jamii husuka, tabia ya
kuuma watu, wapi wanapopendelea kuuma, wapi wanakozaliana kwa wingi na
mazingira yao ya kawaida.
Tafiti hizi zinaanzia Dar es Salaam na
kuhusisha wilaya zote tatu (Ilala, Kinondoni, Temeke). Tafiti
zitaendelea katika baadhi ya mikoa, ikiwa ni pamoja na mikoa 8 ambako
vituo vyetu vipo.Takwimu zitakazopatikana zitaboresha mbinu za kupambana
na ugonjwa huu
(ii)Hatua za Kudumu
WAUJ imeandaa Mpango wa wa namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Homa ya Dengue. Mpango huu kwa kushirikisha sekta mbalimbali.
Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa Dengue
Hitimisho
Wananchi
wanashauriwa kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huu kwani hauambukizwi kwa
kumhudumia mgonjwa au kwa kugusa majimaji yanayotoka kwa mgonjwa. Hata
hivyo tunawashauri wananchi kwenda kwenye vituo vya afya haraka pindi
wanonapo dalili za ugonjwa huu.
Mlipuko wa Dengue unadhihirisha
kuwa mazingira yetu tunayoishi si salama. Ikumbukwe kuwa, kwa sehemu
kubwa, ugonjwa huu unachochewa na mazingira machafu. Aidha mvua hizi
kubwa zinazoendelea zonachangia kuongezeka kwa mazalio ya mbu. Utupaji,
uzoaji na uhifadhi wa taka katika miji yetu hauridhishi kiasi ambacho
kinatoa fursa kwa mazalio ya mbu kuongezeka na hata kuwa karibu zaidi ya
makazi ya binadamu.
Kwa kuwa, hadi sasa hakuna chanjo wala dawa
maalumu kwa ajili ya kudhibiti au kutibu ugonjwa huu, njia kubwa ya
kupambana na ugonjwa huu ni kumzuia binadamu asimwe na mbu. Hivyo basi,
mbinu shirikishi za kutokomeza mbu inabidi zitiliwe mkazo katika
mapambano dhidi ya homa ya Dengue. Njia bora na rahisi ni kuhakikisha
mazalio yote ya mbu yanatokomezwa. Na hili laweza kufanywa na kila mtu
kwa nafasi yake.Tunashauri watu wavae nguo zinazofunika mikono na miguu
na dawa zinazofukuza mbu (mosquito repellent). Tunaelewa kuwa si kila
mtu atakuwa na uwezo wa kununua dawa hizi na ndiyo maana tunakazania
swala la kuangamiza mazalia ya mbu ambalo ni jukumu letu
wote.Tunaendelea kuhamisisha watu na hasa watoto walale ndani ya
vyandarua venye viatilifu wanapolala wakati wa mchana.
Ningependa
kuwakumbusha wananchi wa Tanzania kuwa, huu ni muda muafaka wa
kuzingatia utunzaji bora wa mazingira yetu. Tukitunza mazingira yetu,
nayo yatatutunza na kutuepusha na maradhi yanayoambatana na mazingira
machafu.
0 comments:
Post a Comment