Friday, May 16, 2014

MJUE KWA UNDANI MBU ANAESABABISHA UGONJWA WA DENGUE

MBU Aedes au Aedes aegypti ni wadudu wenye mabawa mawili na miguu sita kutoka familia ya Culicidae.

Mbu huyo asili yake ni Afrika lakini hivi sasa amesambaa sehemu mbalimbali duniani hasa sehemu za tropiko na anapatikana majira yote ya mwaka hasa sehemu zenye maji maji. Machapisho mbalimbali ya kimataifa ya utafiti wa kisayansi kuhusu mbu huyo yanaeleza kuwa amekuwepo kwa zaidi ya miaka milioni 150 iliyopita na kusabisha maradhi kwa binadamu wa kale.

Utafiti wa awali uliofanywa na mwanasayansi Fredric Hasselquist mwaka 1757 ulitaja mbu huyo kwa jina la Culex aegypti. Jina la Aedes aegypti lilianza kutumika mwaka 1920 na lilianzishwa na mwanasayansi Harrison Gray Dyar, Jr. Aedes ni mbu anayeeneza virusi vinavyosababisha ugonjwa maarufu kwa jina na chikungunya, homa ya manjano na homa ya dengue ambayo hivi sasa inaenea kwa kasi katika jiji la Dar es Salaam.

Mbu Aedes ni miongoni mwa wadudu walioko katika hali ya metamofisisi ambao maisha yao hupitia hatua nne zinazowafanya kuwa na tabia na maumbo tofauti ambazo ni yai, lava, pupa na mbu kamili. Unaweza kumtambua mbu huyo kwa kuwa ana mistari meupe miguuni.

Tofauti na mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria ambao huuma usiku, mbu wa homa ya dengue huuma mchana na usiku.Taarifa za kisayansi zinaeleza kuwa mbu jike ndiye hasa anayeuma na kueneza kirusi cha homa ya dengue wakati akifyonza damu katika mwili wa binadamu.

Mbu jike hutumia damu kama lishe kuu ili aweze kurutubisha mayai yake ili kuendeleza kizazi cha mbu hao. Baada ya kunyonya damu ya kutosha mbu jike huweza kutaga mayai 100 hadi 200 kwa uzao mmoja. Jike anaweza kutaga mara tano katika kipindi cha uhai wake.

Mbu aliyepevuka huishi kwa wastani wa wiki mbili hadi mwenzi moja hivyo mbu mmoja aweza kutaga mayai kati ya 500 hadi 1,000 kwa kipindi cha wiki mbili hadi mwenzi mmoja. Wingi wa mayai unategemea kiasi cha damu aliyopata kwa kuwa kadiri anavyopata damu nyingi ndivyo anavyotaga mayai mengi zaidi.

Ingawa mbu huyo anataga mayai 200 katika uzao mmoja, hutaga mayai sehemu tofauti ili kuzuia kizazi chache kisiangamie kwa urahisi endapo adui atavamia mayai hayo. Mayai ya mbu aina ya Aedes yana umbo la mviringo uliochongoka, yana gamba laini na urefu wa milimita moja. Mbu anapotaga hutoa mayai meupe ila baada ya dakika chache hubadilika na kuwa na rangi nyeusi.

Mbu hawa hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba. Mbu huyo anataga kwenye madimbwi ya maji hasa sehemu yenye mafuriko, kwenye mapango ya miti, sehemu zenye mashimo au mapango yaliyotengenezwa na binadamu.

Pia wanataga mayai hao kwenye mapipa, vyungu na makopo ya maua, kweye chupa na makopo yaliyotupwa ovyo, matairi ya gari, vifuu vya nazi, matambara katika viambaza vya nyumba na sehemu zozote zile zenye upenyo hasa katika lundo la uchafu katika viambaza vya nyumba.

Mayai hayo huanguliwa kwa siku tofauti kulingana na hali ya hewa na mazingira ya eneo husika. Sehemu yenye joto kama Dar es Salaam mayai huanguliwa katika siku mbili tu lakini sehemu zenye baridi mayao huchukua hadi siku saba kabla ya kuanguliwa. Mayai ya mbu wa homa ya dengue hayaanguliwi yote kwa wakati mmoja, wakati wa kuanguliwa yanaweza kupishana saa chache au siku nzima kulingana na mazingira ya eneo husika.

Kupishana huko huwezesha kizazi cha mbu kuwepo wakati wote katika majira ya mwaka ikiwa eneo husika litakuwa na hali ya maji maji. Mayai ya mbu anayeeneza ugonjwa wa dengue yanauwezo wa kuhimili hali ya hewa na kukaa muda mrefu bila kuharibika. Ikiwa mayai hayo yametagwa wakati wa kiangazi yanaweza kukaa zaidi ya mwaka mzima bila kuanguliwa kisha huanguliwa kipindi cha mvua ili kiluilui waweza kuishi na kukua vyema.

Kitendo cha yai kukaa muda mrefu kinasababisha changamoto katika harakati za kumuangamiza mbu huyo mwenye uwezo wa kudhuru na hata kuua binadamu ili waweze kuendeleza kizazi chake. Baada ya mayai kuanguliwa viluwiluwi vya mbu huishi kwa kula chembechembe zinazopatikana kwenye maji.

Baadhi ya chembechembe ni ndogo sana haziwezi kuonekana kwa macho bila msaada wa darubini. Viluwiluwi hao huogelea kwenye maji na wakati mwingine huja juu ya maji. Wanaweza kuishi kwenye kina kifupi cha maji ndio maana wanaweza kuzaliana kwenye makopo ya maua yanayoruhusu maji kutwama, kwenye vifuu vya nazi na maeneo mengine yanayohifadhi maji kwa muda mrefu.

Viluwiluwi wanakua kulingana na hali ya hewa, endapo kuna hali joto anaweza kukua kwa muda mfupi katika siku moja ila kama kuna hali ya ubaridi na maji ya kutisha anaweza kubaki kwenye maji hata kwa zaidi ya mwenzi mzima. Lava aliyekomaa huwa na urefu wa milimita nane. Mbu dume hukua haraka zaidi hivyo hubadilika na kuwa mbu kabla ya mbu jike.

Hatua ya kukua yaani yai, lava na pupa huchukua muda mrefu ikilinganishwa na muda ambao pupa anapobadilika na kuwa mbu kamili. Mbu aliyepevuka anaweza kuishi kwa wastani wa wiki mbili hadi mwezi mzima na kusababisha maradhi mbalimbali yanayotokana na homa ya dengue.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Powerade Coupons