skip to main |
skip to sidebar
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amekataa maombi ya
kuwaongezea posho wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) kutoka
Sh150,000 hadi Sh200,000.
Uamuzi huo wa Dk Shein umetokana na hali ya uchumi Zanzibar kutoruhusu nyongeza hiyo kwa sasa.
Katibu
wa BLW, Yahya Khamisi Hamad alithibitisha jana kuwa baraza hilo
lilipeleka kwa Rais Shein maombi la kutaka posho ya vikao hivyo
iangaliwe upya kutokana na sababu mbalimbali, lakini kulingana na
mazingira ya hali ya uchumi ilivyo kwa wakati huu imeshindikana kufanya
hivyo.
Hamad alisema Dk Shein amewataka wajumbe kuwa na subira kwa
kipindi hiki hadi hali itakaporuhusu kiuchumi na suala hilo linaweza
kufikiriwa.
Alisema Dk Shein alitoa msimamo huo alipokutana na Spika
wa baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kwa nia ya kumweleza uamuzi kuhusu
suala hilo. “Rais amekataa maombi ya nyongeza ya posho za vikao vya
wajumbe wa BLW kutokana na hali ya mazingira ya kiuchumi kutokuwa mazuri
kwa wakati huu, amewataka wawe na subira hadi hali ya mambo
itakapotengamaa,” alisema Hamad.
Alisema kamati ya uongozi ya baraza hilo tayari
imekwishataarifiwa kuhusu maombi ya posho kukataliwa na wajumbe wote
kutoka CCM na CUF walitarajiwa kutaarifiwa jana kuhusu uamuzi huo.
Wajumbe hao wamekuwa wakilipwa posho ya Sh 150,000 kwa siku mbali
na mshahara na posho nyingine zinazokaribia Sh4,500,000 kwa mwezi.
Akizungumzia
kikao cha bajeti kinachoanza leo mjini Zanzibar, Hamad alisema kikao
hicho kitalazimika kupunguzwa kwa siku ili kuwahi Bunge Maalumu la
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalofanyika Dodoma ambalo
lipo likizo na linatarajiwa kukutana Agosti 5.
Alisema kwa mujibu wa ratiba, kikao cha bajeti kinatarajia
kutumia siku 56, tofauti na miaka mingine ili kukimbizana na muda na
kuwataka wajumbe kujadili bajeti ili kuokoa muda na kuwahi Bunge la
Katiba.
Aidha, katibu huyo wa BLW alisema kikao hicho kitakuwa na maswali
90, miswada miwili ya sheria ukiwamo wa Sheria ya Fedha na ule wa
Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali mwaka 2014/2015.
Tayari, Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee amesema SMZ katika
mwaka huu wa fedha inatarajia kutumia Sh 705.1 bilioni, kati ya hizo,
makusanyo ya Serikali yatakuwa ni Sh 399 bilioni na kiasi kingine cha Sh
305.3 bilioni ni misaada ya wahisani na mikopo mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment