skip to main |
skip to sidebar
Wakati idadi ya wafungwa ikizidi kuongezeka nchini, Serikali imesema
katika mwaka wa fedha 2014/15 itaendelea kumlisha mfungwa mmoja kwa
Sh500 kwa siku.
Hata kama kiwango hicho cha fedha ni kidogo serikali
inasema kuwa kama idadi ya wafungwa ikiongezeka, inagawanywa na
inawezekana kila mfungwa, kulingana na eneo husika akatumia Sh250 kwa
siku.
Hayo yalielezwa juzi jioni na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias
Chikawe wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge kabla ya kuanza
upitishwaji wa vifungu vya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi kwa mwaka 2014/15.
Wakati Chikawe akieleza hayo, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka wa fedha ulioisha mwaka 2013, inaeleza
kuwa nchini kuna magereza 122 na yanatoa huduma kwa wafungwa 45,000,
wakati uwezo wa magereza hayo ni kuwahudumia wafungwa 22,669.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo chakula cha wafungwa kilitakiwa
kutengewa Sh32 bilioni lakini bajeti iliyoidhinishwa ilikuwa Sh8 bilioni
ikiwa ni pungufu ya Sh24.4 bilioni.
Katika ufafanuzi wake Chikawe
alisema, “Kiwango cha fedha tunachotoa kwa mfungwa na mahabusu kwa siku
ni Sh500. Kiwango hiki ni kidogo ikilinganishwa na gharama halisi za
maisha,” alisema Chikawe na kuongeza;
“Mwaka jana katika mazungumzo na Kamati ya Kudumu ya Ulinzi na
Usalama tulikubaliana kiwango kifike Sh1,500 kwa siku, lakini hali ya
bajeti wakati ule haikukidhi matakwa yetu na hivyo hatukupata kiwango
hicho.”
Alisema hivi sasa wizara hiyo ipo katika mazungumzo na Hazina ili
kuona kama kuna uwezekano wa kupandisha kiwango hicho hadi Sh3,000,
kusisitiza kuwa kama kiwango hicho kikishindikana wataomba hata kupewa
Sh1,500 kwa siku.
“Kuna wakati mahabusu wanakuwa wengi hivyo kiwango cha Sh500 tunachowatengea kinakuwa chini,” alisema.
0 comments:
Post a Comment