skip to main |
skip to sidebar
Kitengo cha kukamata madawa ya kulevya katika uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Mwalimu Nyerere wanafanya kazi ipasavyo baada ya Bibi
mmoja raia wa Nigeria, Olabisi Ibidun Cole (65) amevunja rekodi ya umri
wa watu wanaokamatwa wakiwa na dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Cole alikamatwa Jumatatu
akiwa amemeza kete 82 aina ya heroini zilizokuwa zimefungwa kwenye
karatasi zinazofanana na ganda la sigara, ambazo si rahisi kuonekana
katika mitambo.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na
Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Alfred Nzowa zimesema
pamoja na mbinu zake na kujiamini, mwanamke huyo alikamatwa kutokana na
ushirikiano wa vitengo mbalimbali vya uwanja wa ndege.
Kamanda wa
Polisi wa Uwanja wa Ndege, Hamisi Selemani alisema mwanamke huyo
alikamatwa Mei 19, mwaka huu saa tisa alasiri akijiandaa kwenda Paris,
Ufaransa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.
Selemani
alisema raia huyo aliwasili nchini Mei 15, mwaka huu na alikaa muda wote
bila ya kuwa na shughuli yoyote, jambo ambalo lilitiliwa shaka na
kumkamata.
“Huyu mwanamke achana naye, akisimama mbele yako huwezi
ukaamini kwa jinsi anavyojiamini. Alikuwa na mbinu mpya ya kufunga hizo
kete. Kila moja ilifungwa kwa karatasi inayofanana na ganda la sigara,”
alisema Selemani.
Alisema mwanamke huyo alitumia mbinu hiyo ili asigundulike wakati akikaguliwa kwa mitambo maalumu inayogundua dawa za kulevya.
Taarifa
zaidi zinasema kuwa kutokana na mbinu yake ya ufungaji wa kete,
mwanamke huyo alikuwa tayari amevuka hatua ya kwanza ya ukaguzi.
Nzowa alisema baada ya kumhoji, mtuhumiwa huyo alidai kuwa aliingia nchini kwa ajili ya kutafuta soko la kuuza vipodozi na nguo.
“Wakati
tukiendelea kumhoji, Kikosi Kazi cha Kuthibiti Dawa za Kulevya
kilibaini na kugundua kuwa alikuwa amemeza dawa za kulevya.
“Huyu ni
mzee, lakini tumeshangaa kuona bado ana nguvu za kutosha na tulishangaa
baada ya kutoa kete 20 kwa mara moja katika awamu ya kwanza, jambo hili
si rahisi kutokana na umri wake,” alisema Nzowa.
Mtuhumiwa huyo aliyekuwa na hati ya kusafiria ya Nigeria, anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Nzowa alisema kikosi chake kimejipanga kukabiliana na mbinu zote zinazobuniwa na wanaosafirisha dawa za kulevya.
Takwimu
za kitengo cha dawa za kulevya cha polisi zinaonyesha kuwa kati ya
Januari na Aprili mwaka huu, Cole ni mtu wa 26 kukamatwa katika uwanja
huo na raia wa tano wa kigeni kukamatwa na dawa hizo.
Raia wa kigeni wengine waliokamatwa kutoka nje ya nchi ni kutoka Marekani, Ugiriki, Kenya na Liberia na kesi zao zinaendelea.
0 comments:
Post a Comment